Aliyekuwa mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Ex MT 66807 na wenzake watatu wamehukumiwa kwenda jela miaka 20 baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na meno ya Tembo yenye thamani ya Sh. Mil 198.

Hukumu hiyo imesomwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Kasonde,
Watuhumiwa wengine waliohukumiwa kifungo hicho ni Bakari na Shafii Muhibu Muhibu.

Hata hivyo, Mahakama imemuachia huru Asha Hassan Ulaya, aliyekuwa akishtakiwa na wenzake hao baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka bila ya kuacha shaka yoyote kuwa naye alihusika kwenye tukio hilo.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Kasonde amesema upande wa mashtaka kupitia mashahidi wake nane wameweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao watatu pasipo kuacha shaka yoyote kuwa wametenda kosa.

“Mahakama inawahukumu washtakiwa wote watatu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja kwenye shtaka la kwanza na vilevile shtaka la pili miaka 20,”amesema Hakimu Kasonde.

Pia Mahakama imeamuru meno ya Tembo yarudishwe kwa Mkurugenzi wa Wanyama pori na gari aina ya Suzuki waliyokamatwa washtakiwa waliyotumia kubebea meno hayo itaifishwe na Serikali.
Katika hati ya mashtaka, inadaiwa, Juni 2, mwaka 2016 huko Mbagala Kibondemaji wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote walikamatwa na vipande 10 vya meno ya Tembo.

Pia washtakiwa hao walikuwa wanadaiwa kukubali kisafirisha meno hayo ya Tembo yenye thamani ya Sh. milioni 198, mali ya Serikali ya Tanzania.

Washtakiwa hao wanadaiwa kukutwa na nyara hizo za Serikali bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa wanyama pori.

Tanzania yawasilisha ombi Benki ya dunia
Sosopi ataka adhabu ya Roma Mkatoliki itenguliwe