Kufuatia matukio mbali mbali ya mauaji yaliyokuwa yakiripotiwa nchini, Umoja wa Ulaya ulieleza kusikitishwa na matukio hayo na kutaka uchunguzi wa wazi.
Moja ya matukio hayo ni kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini aliyepigwa risasi Februari 16 eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Marekani katika tamko lake ilieleza kusikitishwa na taarifa za kutekwa na kuuawa kikatili kwa katibu wa Chadema Kata ya Hananasif, Daniel John na kutoa wito wa kufanyika uchunguzi wa uwazi.

Kufuatia hayo, Serikali katika taarifa yake imesema washirika hao hawatambui changamoto za kiusalama na kisiasa ambazo Tanzania imepitia katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

Imesema matamko yao yanatoa tafsiri isiyo sahihi juu ya mwenendo wa siasa na usalama nchini na wakati mwingine yanaleta uchochezi kwa umma na kuchafua taswira ya Tanzania ambayo inatambulika kama nchi ya amani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dkt. Augustine Mahiga inasema ni wazi kwamba wanadiplomasia wana jukumu la kufuatilia na kuripoti matukio ya kisiasa na kiusalama kwenye nchi zao.

Hata hivyo, alisema Serikali ilishangazwa na ukimya wa wanadiplomasia hao wakati wa vitisho vya kiusalama na changamoto ambazo Taifa lilikuwa likipitia wakati wa mauaji ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji.

Pamoja na vyombo vya habari vya ndani kuyapa uzito matukio hayo, Dkt. Mahiga amesema Serikali haikuona ubalozi wowote uliojitokeza kusema neno au kulaani matukio hayo ambayo yalihusisha vifo vya watu.

“Hawa wageni na washirika wetu wanatakiwa kuweka jitihada za kufahamu mazingira magumu yaliyopo nchini badala ya kutoa matamko ya hisia na yasiyothibitishwa ambayo yanaweza kuwa ya kichochezi kwa umma,” amesema Dkt. Mahiga.

Amesema Serikali inakaribisha mazungumzo na washirika hao kwa mambo ambayo watahitaji ufafanuzi ili wafahamu hali halisi.

Balozi Mahiga amesema msimamo wa Serikali ni kuhifadhi taswira ya Taifa ambayo ina historia kubwa kama nchi ya amani na iliyo imara inayozingatia utawala wa sheria, uhuru na demokrasia.

Amesema hatua zinazochukuliwa na Rais John Magufuli za kupambana na rushwa, dawa za kulevya, ukwepaji wa kodi na kusimamia uwajibikaji zimewakasirisha wengi ndani na nje ya nchi hasa ambao walikuwa wananufaika na mfumo uliokuwapo zamani.

Sosopi ataka adhabu ya Roma Mkatoliki itenguliwe
Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Machi 3, 2018