Shirika la afya la Umoja wa Mataifa ulimwenguni WHO, limezindua kampeni mpya ili kuchagiza uelewa na kuchukua hatua kwa ajili ya kuzuia tatizo la kujiua barani Afrika, ambako kuna viwango vikubwa vya vifo vitokanavyo na kujiua.
Kwa mujibu wa takiwimu za shirika hilo zilizotolewa mjini Brazaville, nchini Congo, imesema karibu watu 11 katika kila watu 100,000 wanakufa kila mwaka kwa kujiua Afrika, kikiwa ni kiwango kikubwa zaidi ya kiwango cha wastani cha kimataifa ambacho ni watu 9 kwa kila watu 100,000.
WHO inasema “Hali hii inatokana kwa kiasi kikubwa kwa kutochukuliwa hatua za kushughulikia na kuzuia sababu za hatari ikiwemo hali ya matatizo ya afya ya akili ambayo kwa sasa inaathiri watu milioni 116 likiwa ni ongezeko kubwa kutoka watu milioni 53 mwaka 1990.”
Kampeni hiyo, kupitia mitandao ya kijamii, iliyozinduliwa kabla ya siku ya afya ya akili duniani, inalenga kufikia watu milioni 10 kote kanda ya Afrika, ili kuhamasisha umma, uungwaji mkono wa serikali na watunga sera kwa ajili ya kuongeza umakini na ufadhili wa programu za afya ya akili na juhudi za kuzuia watu kujiua.
Juhudi hizo, ni pamoja na kuwawezesha wahudumu wa afya kusaidia wale wanaokabiliana na fikra za kujiua, kuwaelimisha watu ambao wanaweza kupata fikra hizo juu ya wapi pa kupata usaidizi, pamoja na kuhamasisha umma jinsi ya kutambua na kusaidia wale wanaohitaji msaada kukabiliana na unyanyapaa unaohusishwa na afya ya akili, kifafa, matumizi mabaya ya pombe na madawa ya kulevya.
WHO imesema “Kanda ya Afrika ni maskani ya nchi 6 kati ya 10 zilizo na viwango vya juu vya watu kujiua ulimwenguni na njia zinatotumika zaidi kujiua katika kanda hiyo ni kujinyonga, kunywa sumu na kwa kiasi kidogo kujitosa majini na kuzama, kutumia bunduki, kujirusha kutoka ghiorofani au kumeza madawa kuzidi kiwango.
Dkt. Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema, “Kujiua ni tatizo kubwa la afya ya umma na kila kifo cha kujiua ni janga. Kwa bahati mbaya, hatua za kuzuia kujiua ni mara chache sana kuwa kipaumbele katika programu za afya za kitaifa na tukabiliane na ongezeko la magonjwa sugu na yasiyoambukiza kama vile matatizo ya akili yanachangia kujiua.”