Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka limemfikisha mahakamani mkazi mmoja (46) wa Sombetini Jijini Arusha kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wake (7), mwanafunzi wa darasa la kwanza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo mbali na tukio hilo, pia kwa kipindi cha Januari 2022 – Januari 2023 jumla ya watuhumiwa 241 walipatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela vifungo mbalimbali kwa makosa ya ulawiti na ubakaji.
Amesema, Februari 16, 2023 Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimhukumu Kelvin Wilfred (19), mkazi wa Muriet Arusha kwenda Jela kifungo cha Maisha, kwa kosa la kumbaka mwanafunzi (8), wa darasa la nne.
Kamanda Masejo amesema Mahakama ya wilaya ya Karatu, Arumeru na Monduli ziliwahukumu Peter Leonard (27), Paul Hilonga(60) na John Sanare (24) kwenda Jela vifungo vya maisha kila mmoja kwa makosa ya ubakaji na Elias Ndasikoi (23) mkazi wa Arumeru kifungo cha maisha kwa kosa la ulawiti.
Aidha, Kamanda Masejo amefafanua kuwa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru na Karatu iliwahukumu vifungo vya miaka 30 kila mmoja kwa makosa ya ubakaji James Elirehemma, Elias Robert (27), Japhet Mungure na Theophili Sahalo (32).
Amesema, Jeshi hilo linawashukuru wadau mbalimbali ikiwemo wazazi, viongozi wa Dini, viongozi wa kimila na Waandishi wa Habari kupitia dhana ya ushirikishwaji wa jamii ambayo imepekelekea jamii kuacha kuficha matukio ya ukatili.