Gharama za umeme ni sehemu ya vyanzo vya mgogoro wa kiuchumi kwenye ngazi za familia, hali inayofanya wengi kutafuta namna iwezekanayo ya kudhibiti matumizi ya umeme wakati ambao hawapo nyumbani.
Changamoto hii imegeuka kuwa fursa kwa mwanafunzi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Robert Assay aliyegundua jinsi ujumbe mfupi wa simu (SMS) unavyoweza kutumika kudhibiti matumizi hayo.
Robert, ametumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kugundua namna ambavyo mtumiaji anaweza kutuma SMS akiwa mbali na nyumba yake na ujumbe huo ukasababisha vifaa vinavyotumia umeme kuzima au kuwaka.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum na Dar24 chuoni hapo, Robert alionesha kwa vitendo jinsi ambavyo anaweza kutuma SMS kwa kutumia simu yake ya kiganjani na akapata majibu ya vifaa vyote ambavyo vimewaka na ambavyo vimezimwa (viko – ON/OFF). Kisha, anaweza kutuma SMS ambayo itachagua azime vifaa gani na kuwasha vifaa gani akiwa mbali.
“Ukituma SMS na ukazima taa ambazo ziko wazi kwenye vyumba kama umesahau na vifaa vingine,” alisema.
Aidha, mgunduzi huyo amegundua taa ambazo huwaka wakati wa giza tu, lakini mara panapoanza kupambazuka taa hizo huzima zenyewe. Hali hii inasaidia kudhibiti matumizi ya umeme pasipo na ulazima.
Angalia video yote hapa kuona ugunduzi huo, namna unavyofanya kazi pamoja na ugunduzi mwingine unaomsaidia daktari kutoa huduma: