Kwa mujibu wa kalenda ya matukio, leo dunia inasherehekea ‘Siku ya Baba Duniani’, kwa kiingereza ‘Father’s Day’. Ingawa hakuna sheria ya jinsi ya kuisherehekea, huko Kenya kimetokea kituko cha aina yake, baada ya mwanaume mmoja kuharibu mazao ya shamba kwa hasira kisa mkewe anakwenda kwenye mihangaiko wakati leo ni ‘siku kuu’!

Citizen TV imeripoti mkasa wa mwanaume mmoja mkaazi wa Kaunti ya Kirinyaga aliyeharibu mazao ya shamba yenye thamani inayokadiriwa kuwa Sh. 200,000 za Kenya (sawa na Sh. 4,300,000 za Tanzania), kutokana na hasira alizokuwa nazo baada ya mkewe kuamua kwenda sokoni, licha ya kumsisitiza kuwa leo ni sikukuu muhimu kwake na alipaswa kupumzika nyumbani.  

Mashuhuda wa tukio hilo wameeleza kuwa mwanaume huyo alitumia panga kuharibu ndizi na matunda aina ya parachichi. Majirani wameieleza Citizen TV kuwa mke wa mwanaume huyo ni mfanyabiashara ya mazao ya shamba katika Soko la Kitui.

“Mwanaume huyo alikuwa anataka bibi yake akae nyumbani ndio washerehekee siku ya Father’s Day,” jirani aliyetajitambulisha kwa jina la Muthike alikiambia kituo hicho cha runinga.

Hata hivyo, mazao yaliyoharibiwa sio ya mkewe pekee, bali pia ya wafanyabiashara wenzake, ambao walieleza kuumizwa na kitendo hicho na kwamba wamemfikisha kwa Mamlaka za Serikali ya Kaunti hiyo kwa ajili ya kudai haki yao.

“Mimi ni mmjowa wa wale vitu zao zimeharibiwa, tumefanya uchunguzi tukajua kwamba aliyeharibu ni bwana ya mama mmoja tunaenda na yeye soko,” Hellen Muriithi amesema.

Viongozi wa eneo hilo walithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa wanalifanyia kazi. Majina ya mwanaume huyo na mkewe hayakuwekwa wazi.

Agizo la Serikali kwa Waganga Wakuu wa Wilaya
Israel yatangaza tahadhari kuhusu Rais mpya wa Iran