Katibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Pwani – PUSA, Kelvin Nyambura amewataka Wanafunzi na Wazazi kuwa watulivu akisema vifo hivyo vimewagusa watu wengi na Taifa la Kenya kiujumla na kwamba bado wanafuatilia kuhusu madai ya Dereva kulalamika kuwa basi hilo lilikuwa na tatizo la breki.
Basi la Chuo Kikuu cha Pwani lilipata ajali eneo la kayole kando ya Barabara Kuu ya Nairobi-Naivasha Machi 30, 2023. Picha za Kennedy Amungo I Nation Media Group.
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Pwani umesema ajali hiyo imelikumba basi moja kati ya manne yaliyokuwa kwenye msafara wa wanafunzi 120, madereva wanne na afisa mmoja wa michezo kuelekea kwenye michezo, mjini Eldoret.
Mmoja wa Wanafunzi walionusurika katika ajali hiyo, Ian Okoth (22), alisema “tunataka chuo kikuu kituhakikishie usalama wa magari yetu kabla ya kwenda safari maana tumegundua kuwa dereva alikuwa akilalamika kuhusu breki ya gari.”
Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Kenya, William Ruto amewalilia wanafunzi waliofariki huku akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa, “Rambirambi zetu za dhati kwa familia na marafiki wa wale waliopoteza wapendwa wao kwenye ajali ya Naivasha iliyohusisha basi la Chuo Kikuu cha Pwani. Inasikitisha kwamba baadhi ya walioaga walikuwa vijana wenye mustakabali wenye matumaini. Tunawaombea manusura wapone haraka.”