Watu wanane wamefariki dunia watano wakiwa wa familia moja baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso katika barabara kuu kutoka Lusahunga kwenda Nyakahura wilayani Biharamulo Mkoa wa Kagera.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, William Mwampaghale amesema ajali hiyo imetokea leo Jumanne, Julai 12, 2022 saa saba usiku.
Amesema ajali hiyo imehusisha gari aina ya Mercedes Benz lililokuwa likiendeshwa na Vicent Gakuba (52) raia wa Rwanda, mkazi wa Nyamata Rugesela EAST Province.
Kamanda huyo amesema, gari hilo lilikuwa linakwenda jijiji Dar es Salaam liligongana uso kwa uso na gari aina ya Toyota Succeed lililokuwa likiendeshwa na Nyawenda Bihera Bisalo (35), Muha ambaye ni mkazi wa Lusahunga.
Amesema katika ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wanane ambao ni dreva huyo na abiria wake saba na watano walikuwa wa familia moja.
Amewataja marehemu hao ni Nyawenda Bisalo (35) na Majaliwa Maige (32), mkazi wa Kikoma.
Watano wa familia moja ni ambao ni wakazi wa Nyamalagala ni, Jesca Ntahimula (45), Magreth Kimuna (14), Adidas Sekanabo (12), Zabloni (6) na Vedastina Sekanabo (8) mkazi wa Kikoma.
Amesema katika uchunguzi wa awali wa jeshi hilo umebaini chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari aliyehama kutoka upande wake wa kushoto wa barabara na kuendesha gari upande wa kulia kitendo kilichosababisha kugongana uso kwa uso kwa magari hayo.
Kamanda huyo amesema miili ya watu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Kituo cha Afya Nyakanazi.
Amesema, dereva wa lori, Vicent Gakuba alitoroka baada ya ajali hiyo ila polisi walifanikiwa kumkamata baada ya muda mfupi katika kizuizi cha Kahaza mpakani mwa Tanzania na Rwanda eneo la Rusumo, akiwa katika Lori lililokuwa likielekea nchini Rwanda na atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi kukamilika.