Imefahamika kuwa uongozi wa klabu ya Arsenal bado haujaanza mazungumzo ya mkataba na mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Alexandre Lacazetti.
Meneja wa klabu hiyo ya kaskazini mwa jijini London, Mikel Arteta amesema mazungumzo baina ya pande hizo mbili hayajafanyika, lakini muda utakapowadia yatafanyika, na kila kitu kitakwenda sawa.
Arteta amesema kinachokwamisha mazungumzo ya upande wa uongozi wana mshambuliaji huyo, ni mkakati wa usajili unaoendelea kwa sasa klabuni hapo, lakini anaamini kila jambo lina wakati wake, kwani bado anamuhitaji Lacazetti.
“Ni muda sasa hatujafanya mazungumzo yoyote,” amesema Arteta.
“Bado tuna mambo mengi ya kufanya sokoni na kwenye kipindi hiki, tunaangalia katika mambo yote.
Arteta amesema alimuomba sana Lacazetti, ambaye alitua katika dimba la Emirates akitokea Lyon mwaka 2017, kuendelea kuwa na subra, kwa kufahamu muda si mrefu mambo yake yatakwenda sawa bin sawia.
“Ni mchezaji ambaye ninafurahishwa naye, nadhani tumemuonesha imani yetu kwake tangu nimekua mkuu wa benchi la ufundi,” amesema.
“Lakini hatuwezi kuanza mazungumzo naye, tunajua kila mchezaji aliyebakisha chini ya miaka miwili katika mkataba mara nyingi huanza mazungumzo kama ataendelea au ataondoka.”
Lacazetti ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Arsenal mpaka mwaka 2022 kwa mujibu wa mkataba wake, lakini kumekuwa na sintofahamu juu ya hatima ya mshambuliaji huyo.
Mfaransa huyo alifunga bao lake la 50 katika klabu ya Arsenal kwenye mchezo wa Jumamosi, Septemba 19 dhidi ya West Ham United katika dimba la Emirates na Arsenal kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja.