Tajiri mkubwa barani Afrika Aliko Dangote, bado ana mipango ya kutaka kununua asilimia kubwa ya hisa za klabu ya Arsenal ya Uingereza.

Dangote, ni shabiki mkubwa wa klabu hiyo yenye maskani yake kaskazini mwa jijini London, na aliwahi kuonyesha nia ya kutaka kununua asilimia kubwa ya hisa za klabu hiyo, lakini alikwamishwa na mipango ya bosi wa sasa Stan Kroenke baada ya kuzidiwa kete.

Dangote raia wa nchini Nigeria anakadiriwa kuwa na utajiri wa Pauni Bilioni 8.3, na ndani ya miaka minne ijayo amejizatiti kutimiza lengo la kuwa mtu mwenye kauli ya mwisho ndani ya klabu ya Arsenal.

“Labda miaka mitatu mpaka minne ijayo, ninaweza kutimiza lengo la kumiliki asilimia kubwa ya hisa za klabu ya Arsenal. Nahitaji kupata muda wa kutosha ili nijipange na mpango huo kwani ninafahamu huenda ikawa ni changamoto kubwa dhidi ya wapinzani wangu kibiashara ambao tayari wanamiliki hisa klabuni hapo. Alisema Dangote alipohojiwa na tovuti ya Bloomberg

“Sina mipango ya kumiliki asilimia kubwa ya hisa za Arsenal halafu mambo yakaendelea kama ilivyo sasa, ninahitaji kubadilisha kila kitu ili kuleta mafanikio kama ilivyo kwa klabu nyingine za barani Ulaya.” Aliongeza Dangote

Mfanyabiashara kutoka nchini Marekani Stan Kroenke, bado anamiliki asilimia kubwa ya hisa za klabu ya Arsenal na ameonyesha kumkubali meneja Arsene Wenger ambaye anadaiwa kukwamisha mafanikio ya kutwaa mataji, kwa kufanya usajili wa wachezaji ambao wanashindwa kupambana na vikosi vya klabu nyingine za Uingereza na barani Ulaya.

Vipengele vya MTV MAMA vyatajwa, wasanii wachache TZ kushiriki
Mtego Wa Mauricio Pochettino Wamnasa Danny Rose