Wananchi wa Guinea ya Ikweta, hapo kesho Jumapili Novemba 20, 2022 wanatarajia kufika kwenye vituo vya kupigia kura ili kushiriki uchaguzi wa kumpata Rais wa nchi hiyo, ambapo Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo aliyeitawala nchi hiyo tangu Agosti mwaka 1979 anatarajiwa kushinda muhula wa sita wa uchaguzi huo.
Utawala wa kiongozi huyo unajulikana kwa ukandamizaji wa wapinzani na kushuhudia majaribio kadhaa ya mapinduzi, huku chama kimoja pekee cha upinzani kikipitishwa kuweka mgombea wa kiti cha Urais wa nchi hiyo.
Nguema mwenye umri wa miaka 80, amekaa madarakani kwa miaka 43 na utawala wake ndio mrefu zaidi katika viongozi waliokaa muda mrefu madarakani walioko hai duniani, ukiwaondowa watawala wa kifalme.
Kiongozi huyo, alitwaa madaraka kutoka kwa Francisco Macias Nguema ambaye mwaka 1968 aliingia madarakani kama rais wa kwanza wa Guinea, baada ya uhuru kutoka Taifa la Uhispani na baadae kujitangaza binafsi kuwa rais wa maisha.