Mshambuliaji kutoka nchini England, Andy Caroll huenda akarejea katika benchi la majeruhi la klabu ya West Ham Utd, kufuatia sintofahamu iliyoibuka usiku wa kuamkia hii leo wakati wa mchezo wa ligi kuu ya soka dhidi ya Bournemouth.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miakam 27, amekua akiandamwa na majeraha ya mara kwa mara na hufikia hatua ya kukaa nje ya uwanja kwa ajili ya kujiuguza kwa zaidi ya miezi miwili hadi mitatu.

Katika mchezo wa usiku wa kuamkia hii leo, Caroll, alipata dhoruba katika dakika ya 15, kufuatia maumivu ya misuli hali ambayo iliwalazimu madaktari wa timu kuingia uwanjani na kuanza kumtibu.

Hata hivyo hakufanikiwa kuendelea na mchezo huo, kutokana na kulazimika kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Nikica Jelavic katika dakika ya 15.

Mpaka sasa haijafahamika ni lini Caroll ataweza kurejea uwanjani kuendelea na majukumu ya kuisaidia klabu yake ya magharibi mwa jijini London, lakini kilichotawala miongoni mwa viongozi na mashabiki wa klabu hiyo ni kukosekana kwake kwa kipindi kingine cha majuma kadhaa yajayo.

Ni siku chache zimepita, ilishuhudiwa Carroll akirejea katika majukumu yake uwanjani baada ya kupona majeraha ya goti ambayo aliyapata mwezi Februari mwaka 2015.

Katika mchezo wa jana West Ham Utd walifanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Bournemouth.

Mabao ya wagonga nyundo wa jijini London ambao walikua ugenini, yalipachikwa wavuni na Dimitri Payet pamoja na Enner Valencia aliyefunga mara mbili huku bao la wenyeji likikwamishwa wavuni na Harry Arter.

Jurgen Klopp Ashangazwa Na Meneja Wa Arsenal
Njonjo Amaliza Tetesi Ajiunga Na Newcastle Utd