Meneja wa klabu ya Liverpool, Jurgen Klopp amekiri kushangazwa na meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger, kutokana na utendaji wake wa kazi kwenye ligi kuu ya soka nchini England.

Klopp, ameonyesha kushangazwa na mzee huyo kutoka nchini Ufaransa, alipozungumza na vyombo vya habari kuelekea katika mchezo wa ligi ya nchini England, ambapo hii leo majogoo wa jiji Liverpool watakua nyumbani wakiwakabili Arsenal.

Klopp, amesema kwa kipindi kirefu amekua akiifuatilia ligi ya nchini England na amebaini Wenger, ni mtu mwenye uvumilivu uliopitiliza kutokana na mazingira ya ushindani wa soka la nchini humo.

Amesema kuendelea kukaa kwake madarakani kama mkuu wa benchi la ufundi la Arsenal, kunathibitisha mambo mengi ambayo amekua akikutana nayo lakini kwa wakati mwingine huyachukuliwa kama changamoto ya kuendelea kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Hata hivyo Klopp ambaye alichukua kijiti cha kuiongoza Liverpool baada ya kutimuliwa kwa Brendan Rodgers, amekiri kumuheshimu na kumpenda Arsene Wenger kutokana na mwenendo wake wa ufundishaji wa soka.

Arsene Wenger anaendelea kuwa meneja wa kipekee katika ligi ya nchini England kutokana na sifa ya kukaa kwenye ligi hiyo kwa zaidi ya miaka 20 bila kufukuzwa wala kuhamia kwenye klabu nyingine.

ISIS watajwa shambulizi la kujitoa mhanga Liloua Wageni
Andy Caroll Azusha Hofu Kubwa West Ham United