Mwanamume ambaye bado hajatambulika anatafutwa na Polisi akidaiwa kumshambulia Daktari na nesi wa zamu  katika Hospitali ya huduma za Mama na Mtoto ya Akure iliyopo Jimbo la Ondo nchini Nigeria, akiwatuhumu kuhusika na kifo cha mwanawe (5).

Kisa hicho, kinadaiwa kutokea Jumamosi Machi 25, 2023 wakati mwanamume huyo alipompiga Daktari na Muuguzi huyo wa zamu kwa makofi na kuwakimbiza Wahudumu wengine hali iliyosababisha huduma za  Hospitali hiyo ya Serikali kusimama kwa saa kadhaa.

Baada ya tukio hilo, mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa aliondoka akiwa amebeba mwili wa mwanae kwa hasira  ambapo wahudumu wengine waliripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Tarafa ya Akure, lakini Askari wa zamu alisema hawawezi kumkamata mshambuliaji kutokana na kukosa usaidizi.

Mashuhuda wa tukio wamesema, ”huyo Mwanamume na mkewe walimkimbiza mtoto wao katika wodi ya dharura huku wakipiga kelele za kuomba msaada, ili kuokoa maisha yake ambaye alikuwa na hali mbaya, wauguzi wote wa zamu walimsaidia na mtoto akalazwa kisha Baba yule aliambiwa alipe kiasi cha Naira 8,000 lakini kwa bahati mbaya wakati wa mchakato huo mtoto alifariki.”

“Alipofahamishwa kuwa kijana wake amefariki, kwa hasira alikimbilia ndani ya gari lake na kutoa panga ambayo aliitumia kumpiga nesi na daktari wa zamu. Alikuwa amekasirika kweli. Kwa hiyo kila aliyekuwa zamu alilazimika kuokoa usalama wake,” alisema Ojuku Uche mmoja wa mashuhuda.

Wakithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya Madaktari, Mkuu wa Serikali Jimbo la Ondo na Madaktari wa Meno, kwa nyakati tofauti walilaani shambulio hilo  huku Chama cha Madaktari  kikikanusha ripoti kwamba wafanyikazi wa zamu hawakumtilia maanani mgonjwa.

Katika taarifa iliyotolewa na mwenyekiti na katibu wa Jumuiya hiyo, Dkt. Makinde Olugbenga na Dkt. Adeniyi Adetayo wamesema Madaktari walijitahidi kuokoa maisha ya mgonjwa na haikuwezekqna huku Ofisa Uhusiano wa Polisi, Funmilayo Odunlami akisema bado hajafahamishwa kuhusu tukio hilo.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Machi 27, 2023
Sloti ya Forest Rock| Ushindi upo kwa Wanyama Pori