Shirikisho la soka Tanzania (TFF), limeendelea kutoa shukurani kwa mashabiki wa soka nchini waliojitokeza uwanja wa taifa, pamoja na wale walioufuatilia mchezo wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kuwania nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia kati ya Taifa Stars dhidi ya Burundi.
Taifa Stars ilishinda mchezo huo kwa changamoto ya mikwaju ya penati tatu kwa sifuri, baada ya matokeo ya jumla ya mabao mawili kwa mawili, yaliyopatikana katika michezo miwili iliyochezwa mjini Bujumbura na Dar es salaam.
Katibu mkuu wa shirikisho hilo Wilfred Kidao ametoa shukurani hizo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika hii leo jijini Dar es salaam, sambamba na kamati ya hamasa.
“Kwanza kabisa niwapongeza mashabiki kwa kazi kubwa ya kuiunga mkono Taifa Stars waliyoifanya dhidi ya Burundi, hakika ilikuwa ni ya aina yake na ambayo sikuwahi kuiona.
“Hata hivyo, baada ya mchezo wetu na Burundi, tunajipanga kwa ajili mchezo ujao wa CHAN dhidi ya Sudan, ambao tutaucheza hivi karibuni.
“Tukifanikiwa kuwatoa Sudan tutakwenda katika fainali hizo na tutakuwa tumeandika historia ya kushiriki fainali zote kubwa za Afrika ndani ya kipindi kifupi,” alisema Kidau.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Hamasa ya Taifa Stars, Haji Sunday Ramadhan Manara amesema: “Kwa upande wa kamati yetu tumejipanga vizuri kwa ajili ya kutimiza majukumu ya kitaifa, lakini pia niwaombe Watanzania wote kuendeleza utamaduni wa kuja kwa wingi uwanjani, kwa ajili ya kuiunga mkono timu yetu ya taifa.
“Tulichofanya dhidi ya Burundi basi kiwe mara mbili zaidi tutakapokutana na Sudan hivi karibuni katika Uwanja wa Taifa,” amesema.
Kikosi cha wachezaji wa ndani cha Taifa Stars kinatarajiwa kuingia kambini juma lijalo jijini Dar es salaam, kwa maandalizi ya mchezo ujao wa kuwania kufuzu fainali za mataifa bingwa ya Afrika (CHAN) dhidi ya Sudan.
Mchezo wa mkondo wa kwanza baina ya timu hizo umepangwa kuchezwa septemba 20, huku mchezo wa mkondo wa pili utaunguruma mjini Khartoum Oktoba 18.