Baadhi ya wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Ayoub Bakar Hamad na Nasoro Hamis Mohamed wametangaza kutokubaliana na uamuzi uliofanywa na mwenyekiti wa Tume hiyo, Jecha Salim Jecha wa kufuta uchaguzi mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wakiongea jana kupitia ‘Sauti ya Amerika (VOA), wajumbe hao walieleza kuwa hawakuhusishwa na mwenyekiti wao katika maamuzi aliyoyatangaza.

“Hiyo ni kusema kwamba maamuzi aliyotoa mwenyekiti wa Tume ni maamuzi yake binafsi, sio maamuzi ya Tume na sio maamuzi ya Tume ya Uchaguzi,” alisema Ayoub Bakar Hamad.

Alieleza kuwa alichokifanya Mwenyekiti wa Tume hiyo hakitokani na maamuzi ya kikao cha Tume hivyo ni kinyume cha katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Mwenyekiti hakutushirikisha sisi, hakutusimulia wala hakutuachia maelekezo yoyote juu ya taarifa hizo. Kwa hiyo natangaza mimi na mwenzangu kwamba alichokifanya mwenyekiti wetu sisi hatukifahamu wala hatuhusiki, ni maamuzi yake binafsi.”

Botswana Watoa Hifadhi Kwa Wachezaji Wa Eritrea
Profesa Lipumba Azungumzia Uamuzi Wa ZEC Kufuta Uchaguzi