Leo ni kumbukizi ya kuzaliwa kwa Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyezaliwa Aprili 13, 1922 katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma, Mkoa wa Mara, Tanzania.

Julius alikuwa ni mmoja wa watoto 26 wa Chifu wa kabila la Wazanaki, Mzee Nyerere Burito na katika utoto wake alichunga mifugo ya baba yake hadi alipofikisha umri wa miaka 12 ambapo alianza Shule akitembea kilomita 30 hadi Musoma.

Baada ya kumaliza Shule ya Msingi aliendelea kusoma Shule ya Wamisionari Wakatoliki huko Tabora na alipofikisha miaka 20, alibatizwa akawa Mkatoliki huku Mapadre wakibaini kipaji alichonacho na wakamsaidia kusomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Kampala, Uganda kuanzia 1943 hadi 1945.

Akiwa Makerere alianzisha Tawi la Umoja wa Wanafunzi Watanganyika na pia akajihusisha na Tawi la Tanganyika African Association (TAA) na baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora akawa Mwalimu katika Shule ya Sekondari ya St. Mary´s.

Mwaka 1949, alipata nafasi ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh huko Uingereza Shahada ya Uzamili ya Historia na Uchumi na kuhitimu mwaka 1952 akiwa Mtanzania wa kwanza kusoma katika Chuo Kikuu cha Uingereza na Mtanzania wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanzania.

Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Tanganyika African Association (TAA), Chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Makerere. Mwaka 1954 alikibadilisha Chama cha TAA kuwa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) ambacho kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko cha TAA.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, Chama cha TANU tayari kilikuwa chama cha siasa kinachoongoza Tanganyika. Uwezo wa Mwalimu Nyerere uliwashtua viongozi wa kikoloni na kumlazimisha achague kufanya kazi ya siasa au abaki na kazi ya ualimu. Nyerere alisikika akisema kuwa alikuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.

Alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchini Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta muungano katika kupigania Uhuru. Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Baraza la Udhamini na Kamati ya Nne ya Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani.

Uwezo wake wa kuunganisha watu ili wawe na umoja na mshikamano kutetea haki zao pamoja na kipaji chake cha kujenga hoja, kutetea na kuzungumza kwa ufasaha ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata Uhuru bila umwagaji wa damu. Ushirikiano mzuri aliouonyesha kwa aliyekuwa Gavana wa wakati huo, Bw. Richard Turnbull ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa Uhuru.

Tanganyika ilipata Uhuru wake tarehe 9 Desemba, 1961 na Nyerere alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika huru. Mwaka mmoja baadaye, Nyerere alikuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika. Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika kuleta Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyounda Tanzania baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 ambayo yalimtoa madarakani Sultani wa Zanzibar, Jamshid bin Abdullah.

Mnamo tarehe 5 Februari, 1977 Mwalimu Nyerere aliongoza chama cha TANU katika kuungana na chama tawala cha Zanzibar cha Afro – Shiraz Party (ASP) na kuanzisha Chama kipya kilichoitwa Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa Mwenyekiti wake wa kwanza.

Mwalimu Nyerere aliongoza Taifa kwa miaka 23 hadi mwaka 1985 alipostaafu na kumwachia nafasi Rais wa Awamu ya pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi. Yeye alibaki kuwa Mwenyekiti wa CCM hadi mwaka 1990 alipostaafu licha ya kuwa aliendelea kuwa na heshima kubwa katika nyanja za siasa ya Tanzania na duniani hadi kifo chake.

Mwalimu Nyerere alitumia muda mwingi kukaa kijijini kwake Butiama huku akilima shambani kwake. Pamoja na hayo, alianzisha Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation mwaka 1996. Aidha, alikuwa mpatanishi wa vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Burundi. Pia kati ya mwaka 1987 hadi 1990 alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini.

Tarehe 14 Oktoba 1999, ni siku ambayo Taifa la Tanzania halitaisahau kamwe kwani Mwalimu Nyerere aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 77 katika Hospitali ya St. Thomas iliyoko jijini London, Uingereza baada ya kuugua kansa ya damu. Mwili wa Mwalimu ulipokelewa jijini Dar es Salaam tarehe 18 Oktoba, 1999 na kupelekwa nyumbani kwake Msasani.

Tarehe 20 Oktoba, 1999 mwili wa Baba wa Taifa ulipelekwa Uwanja wa Taifa ili Watanzania kwa ujumla waweze kumuaga mpendwa wao. Tarehe 21 Oktoba, 1999 ilifanyika sala ya mazishi ya Kitaifa katika uwanja huo ambayo iliongozwa na Muadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walihudhuria ibada hiyo. Watu waliendelea kumuaga Baba wa Taifa Taifa usiku na mchana hadi tarehe 22 Oktoba, 1999 jioni mwili wake ulipoondolewa na kusafirishwa kwenda Musoma na hatimaye ukasafirishwa kwenda kijijini kwake Butiama kwa ajili ya mazishi.

Mazishi ya Mwalimu Nyerere yalifanyika tarehe 23 Oktoba, 1999 nyumbani kwake huko Mwitongo katika kijiji cha Butiama, wilayani Musoma Vijijini, mkoani Mara na kama angekuwa hai basi leo hii angekuwa anatimiza umri wa miaka 101. ENDELEA KUPUMZIKA KWA AMANI BABA WA TAIFA – MWL. JULIUS KAMBARAGE NYERERE.

Elias Maguri mambo safi Geita Gold FC
Ahmed Ally: Tunahitaji ushindi ili tuwakumbushe status yao