Balozi wa Tanzania nchini Malta, mwenye makazi yake Roma nchini Italia, Mahmoud Thabit Kombo amewasilisha hati za utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Malta, Dkt. George Vella Ikulu ya Malta.
Baada ya kuwasilisha hati hizo, pia walizungumza mambo mbalimbali wakiakisi kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kisiasa na azma ya nchi ya Malta kuwa daraja baina ya Afrika na Umoja wa Ulaya.
Aidha, pia walisisitiza suala la kuibua fursa zenye manufaa kwa pande zote mbili katika maeneo ya elimu, utalii, utamaduni, uvuvi, usafiri wa majini, biashara na uwekezaji.
Uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Malta, ulianza mwaka 2015 na tangu wakati huo, juhudi za kuukuza zimekuwa zikifanyika kupitia sekta za elimu, utalii, usafiri wa anga na kupitia majukwaa ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola ambazo nchi zote mbili ni wanachama.