Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amemuaga Balozi wa Australia nchini mwenye makazi yake nchini Kenya, Luke Williams baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi.
Akizungumza na Balozi Williams walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Waziri Mbarouk amesema Tanzania na Australia zimekuwa na uhusiano mzuri uliowezesha mataifa hayo kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za elimu, utalii, madini, nishati, mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na biashara na uwekezaji.
Waziri Mbarouk ameongeza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Australia ni jambo lililochochewa na kazi nzuri iliyofanywa na Balozi Williams wakati akitekeleza majukumu yake ya kibalozi na kusema katika kipindi chake ameiwakilisha vyema Australia na kuonesha mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa kati ya Tanzania na Australia.
Amesema, “kazi yako imechochea uboreshaji wa sekta za elimu, utalii, madini, nishati, uchumi wa buluu na kuchangia ukuaji wa sekta ya biashara uwekezaji katika nchi zetu, ni matumaini yangu kuwa utaendelea kuwa Balozi mwema kwa Tanzania nchini Australia na kokote uendako Duniani.”
Kwa upande wake Balozi Williams, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano iliomuonesha wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake ya kibalozi. “Kwa kweli ni ngumu sana kuaga lakini haya ndiyo Maisha ya wanadiplomasia hakuna budi, siku zote nitakumbuka utu na ukarimu wa Watanzania,” amesema Williams.
Balozi Williams ameihakikishia Tanzania kuwa Australia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha inaboresha zaidi sekta za elimu, utalii, mabadiliko ya tabianchi, uchumi wa buluu pamoja na biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote mbili.