Uhusiano kati ya Nchi ya Misri na Zanzibar umeendelea kukua na kuimarika licha ya Serikali ya Misri kufunga Ubalozi wake mdogo Zanzibar kwenye miaka ya 1990.

Hayo yamesemwa Bungeni hii leo Oktoba 31, 2023 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Shaurimoyo, Ali Juma Mohamed aliyetaka kujua sababu za nchi ya Misri kufunga Ubalozi wake Mdogo Zanzibar.

Akijibu swali hilo, Balozi Mbarouk amesema Misri haikutoa sababu za kufunga Ubalozi wake mdogo Zanzibar na kudai kuwa pamoja na kufungwa kwa ofisi hizo, mahusiano na ushirikiano kati ya Misri na Zanzibar yameendelea kukua na kuimarika siku hadi siku kupitia Ubalozi wake uliopo Dar es Salaam.

Awali, katika suala lake la msingi, Mohamed alitaka kujua idadi ya Balozi ndogo zilizopo Zanzibar, ambapo alijibiwa kuwa hadi kufikia Agosti, 2023, nchi zilizofungua Ofisi ndogo za Ubalozi Zanzibar ni China, India, Msumbiji, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu – UAE.

Aidha, Naibu Waziri alieleza kuwa suala la kufungua na kufunga Ubalozi ni suala la kawaida katika ulimwengu wa Kidiplomasia.

Alitaja sababu za nchi kufunga Ubalozi kuwa ni pamoja na kutetereka au kuharibika kwa mahusiano ya nchi husika, nchi kubadili mwelekeo wa kimaslahi na kistrategia, kukosekana kwa usalama katika nchi husika na hali ya kiuchumi, ambapo nchi hufunga Ubalozi au Konseli Kuu kwa ajili ya kubana matumizi.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Novemba 1, 2023
DCEA yawauma sikio Wazee wa Kimila vita Dawa za Kulevya