Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Innocent Bashungwa amezindua vifaa maalum kwaajili ya utafsiri wa lugha vilivyonunuliwa na serikali kwa gharama ya shilingi Milioni 187.5 ikiwa ni mpango wa kuendeleza ukuaji wa lugha ya kiswahili hususani kimataifa.
Ameyasema hayo leo Agosti 21,2021 Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, huku akilisisitiza Baraza la Kiswahili Tanzania BAKITA kutumia fursa iliyo mbele yao na kujenga mfumo wa kuwatambua wataalam wa kiswahili waliopo nchini.
Ameongeza kuwa wakati huu ni muafaka ambapo mataifa mengi hususani yaliyopo ndani ya Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) yanatafuta wataalamu wengi kwa ajili ya kufundisha na kutafsiri lugha ya kiswahili.
“Baraza la Kiswahili la Taifa(BAKITA) linatakiwa kwenda na teknolojia kwa kutengeneza mfumo maalumu wa utambuzi wa wakalimani ili kurahisisha upatikanaji wa ajira zao katika mataifa mbalimbali,”. Amesema Bashungwa
Aidha Waziri Bashungwa amesema ni muhimu kuwa na utaratibu huo utakaotokana na mfumo huo na kwamba hata kama kuna changamoto ya kuutengeneza mfumo huo Wizara yake ipo tayari kuwasiliana na Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili kuwasaidia wataalamu kufanikisha suala hilo.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji Mkuu wa BAKITA Consolatha Mushi ameishukuru Serikali kwa msaada wa vifaa hivyo, ambapo ununuzi wa vifaa hivyo utawawezesha watu mbalimbali kujifunza lugha ya ukalimani sambamba na kuongeza idadi ya watafisiri wa lugha nchini.