Watu 22, abiria wa basi la kampuni ya Isamilo Express likitokea Mbeya kwenda Mwanza wamepata ajali baada ya gari hilo kuacha njia na kupinduka.
Taarifa iliyotolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, SACP Ulrich Matei imeeleza kuwa ajli hiyo imetoke mnamo tarehe 10.09.2020 majira ya saa 06:40 asubuhi maeneo ya Inyala – Mablock, kata ya Inyala, tarafa ya Tembela, wilaya ya Mbeya vijijini, mkoa wa Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya – Njombe.
Kamanda Matei ameeleza kuwa ajali hiyo imehusisha gari lenye namba ya usajili T.629 CQC Scania likiendeshwa na Dereva aitwaye Kini Daud Malimi (51), mkazi wa Igoma Mwanza ambalo liliacha njia, kupinduka na kusababisha majeruhi na uharibifu wa Gari hilo na baadhi ya mali za abiria.
Katika ajali hiyo abiria 22, wamepata majeraha sehemu mbalimbali kati yao 12 ni wanaume na 10 ni wanawake, ambapo majeruhi 08 kati yao wanaume 05 na wanawake 03 wamepelekwa hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya na wengine 14 kati yao saba wakiwa ni wanaume na saba ni wanawake, wanaendelea kupatiwa matibabu kituo cha afya Inyala.
Kwa mujibu wa SACP Matei, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kutaka kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari pamoja na mwendo kasi katika eneo lenye mteremko mkali.