Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema katika stadi za ujasiriamali vazi la Batiki litawekewa viwango ili mtu yeyote Duniani akishika vazi hilo itambulike imetoka Tanzania.

Waziri Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo Julai 08, 2022, wakati wa Siku ya vazi la Batiki ambayo imefanyika kwenye Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam wakati wa Maonesho ya 46 ya Biashara yanayoendelea.

“Tunataka mahali popote vazi hili la Batiki mtu akilishika ijulikane kuwa ni Batiki ya Tanzania kwani ni kwa njia hiyo tutaweza kuwakomboa watu wetu na Umasikini,” amesema Dkt. Gwajima.

Vazi la Batiki katika mitindo mbalimbali

Ameongeza kwamba, lengo ni kuwafikia watengenezaji wa Batiki wakiwemo Wanawake walio wengi kwenye Sekta ya Biashara ndogo ndogo ili kila mmoja aweze kuinuka kiuchumi.

Dkt. Gwajima amesema kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan amefungua fursa kwa Wanawake na kuwaonesha kuwa wanaweza, hivyo nimuhimu kuchapa kazi kwa kushirikiana na Wanaume kuinua Uchumi wa Nchi.

“Kutungwa kwa Sheria ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka 2018 inayozitaka Halmashauri zote kutenga 10% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa makundi maalum ikiwemo wanawake imewasaidia wengi,” alisema Dkt. Gwajima.

Batiki

Ameongeza kuwa, mwaka 2020/21 zilitengwa jumla ya Sh. Bil. 62.68 na kufikia 30th Juni, 2021 Sh. Bil. 53.81 zilikopeshwa kwa Vikundi 7,993 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu sawa na asilimia 86.

Amebainisha kuwa, kati ya Fedha hizo Sh. Bil. 28.17 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake 4,894 vilivyozalisha ajira 52,428.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe amewahimiza waandaaji wa Siku ya Batiki kufanyika nchi nzima.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Zainab Chaula ameahidi kushirikiana na Katibu Mkuu wa Zanzibar kufanyia kazi maelekezo ya Mawaziri hao.

Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania Latifa Mohamed Khamis, aliomba Serikali kuhakikisha Shirika la Viwango nchini TBS, wanatoa Vyeti vya Ubora wa Bidhaa za Batiki.

Waajiri wahimizwa kuchangia WCF kwa wakati
Habari kuu kwenye magazeti ya leo Julai 9, 2022