Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limeishauri Kamati Kuu ya Chadema kuwafukuza uanachama, wanachama 19 waliokwenda kinyume na msimamo wa chama hicho, kwa kukubali uteuzi wa ubunge viti maalumu.
Hayo amesema Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu leo Novemba 26, 2020, wakati anazungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambapo alitoa msimamo wa baraza hilo, baada ya kamati tendaji kukutana katika mkutano jana usiku Jumatano kwa njia ya mtandao kujadili wanachama hao 19 waliokwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum.
Akitangaza maazimio ya kamati tendaji hiyo ya Bavicha, Pambalu amesema, baraza hilo linaishauri kamati kuu hiyo ya Chadema kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wabunge hao viti maalumu.
“Ziko adhabu nyingi za kuchukuliwa kwa hao 19, kuvuliwa nyadhifa zao, kunyang’anywa uanachama wao, dhambi ya usaliti ni dhambi mbaya, hatutaki kushinikiza Kamati Kuu ichukue hatua gani, lakini hatua kali zichukuliwe ikiwemo kuwafukuza uanachama wao,”amesema Pambalu.
Wanachama hao 19 wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA), Halima Mdee, waliapishwa kuwa wabunge viti maalumu na Spika Job Ndugai, tarehe 24 Novemba 2020, kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma.