Rais wa Marekani Joe Biden ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kina ili kutambua chanzo cha maambukizi ya virusi vya corona.
Katika taarifa yake Biden amesema wengi kwenye mashirika ya ujasusi ya Marekani wanaamini kuna uwezekano wa aina mbili, kwamba binadamu aliambukizwa virusi hivyo na mnyama aliyeathirika navyo, au vilisambaa baada ya kutokea ajali kwenye maabara.
Biden amesema hakuna ushahidi wa kutosha wa kuupa uzito uwezekano mmoja kuliko mwingine.
Aidha Rais huyo amesema maabara za kitaifa za Marekani zinapaswa kusaidia katika uchunguzi na ameitolea wito China kushirikiana wachunguzi wa kimataifa huku akitarajia matokeo ndani ya siku 90.
“Tutaendelea kushinikiza kufanyika uchunguzi wa kimataifa juu ya chimbuko la virusi vya corona nchini China, na tutaendelea kuishinikiza China kushiriki kikamilifu katika uchunguzi huo, unaohitajika kuvielewa zaidi virusi ambavyo vimechukua maisha zaidi ya watu milioni 3 kote ulimwenguni,” amesema Naibu Katibu wa Wanahabari wa Ikulu ya White House, Karine Jean-Pierre.