Bilionea kutoka China, Mkurugenzi mtendaji na mwanzilishi wa Kampuni ya Alibaba, Jack Ma, ametangaza kustaafu majukumu yake kwenye kampuni hiyo ambayo alianzisha yeye na wenzake 18 miaka 20 iliyopita.
Jack Ma amestaafu nafasi hiyo baada ya kutimiza umri wa miaka 55 na sababu kubwa iliyomfanya kuachia ngazi anasema ni kuruhusu uwezo wa vijana kujionesha kwa kuiongoza kampuni hiyo kwa sababu anaamini amewafundisha mengi hivyo anataka kuona uwezo wao wa kuisogeza Kampuni hiyo inayotajwa kuingiza kipato kikubwa Duniani.
Kampuni ya Alibaba ilianzishwa miaka 20 iliyopita kwa mtaji wa Tsh.Milioni 138 lakini kwa sasa ina thamani ya Tsh. Trilioni 966 huku Jack Ma akitajwa kuwa na utajiri wa Tsh. Trilioni 92.
Kabla ya kuanza biashara Jack Ma amewahi kuwa Mwalimu na amesema anataka kurudi tena kufundisha pia kuhakikisha anatoa misaada ya kutosha kwaajili ya kusaidia jamii.
Jack Ma anasema anategemea kuona Kampuni hiyo ikiendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwaajili ya kusaidia jamii pia kuhakikisha ina boresha masuala ya teknolojia kama mapinduzi ya 5G pamoja na akili bandia (Artificial Intelligence).
“Sio rahisi kuwa na Kampuni yenye nguvu lakini ni ngumu zaidi kuwa na Kampuni nzuri,” alisema.
“Kampuni yenye nguvu hutajwa kutokana na uwezo wake wa kiuchumi lakini Kampuni nzuri ni ile inayowajibika na yenye ustaarabu,” aliongeza zaidi.
Alibaba ni Kampuni inayojishughulisha na biashara mbalimbali kama masuala ya kiteknolojia, biashara mtandaoni, utengenezaji wa vifaa mbalimbali vya teknolojia na uwekezaji.