Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 42 kuboresha kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Kiloleni, wilaya ya Tabora mjini, mkoani Tabora ili kuimarisha huduma ya umeme.
Akizungumza alipotembelea kituo hicho Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amesema kuwa, Tabora ni Mkoa wa kimkati wenye fursa nyingi za maendeleo ikiwemo migodi, kilimo na viwanda hivyo, unahitaji kuwa na umeme wa uhakika kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa kasi.
Ameongeza kuwa, umeme wa uhakika mkoani Tabora utawezesha uendeshaji wa train ya kisasa (Standard Gauge) ambayo uzinduzi wa shughuli za ujenzi wake unatarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Aidha, Naibu Waziri Byabato amebainisha kuwa, Kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Kiloleni ni miongoni mwa vituo 9 vinavyotarajiwa kuboreshwa mkoani Tabora ili kuwa na umeme wa uhakika.
Sambasamba na hayo Naibu Waziri Byabato, ameagiza kutengenezwa kwa transfoma iliyoharibika ndani ya Mwezi Julai, 2021 ili kuongeza nguvu ya umeme kituoni Kiloleni licha ya kuwa kuna transfoma moja inayofanya kazi.