Mgombea wa urais nchini Uganda Robert Kyagulanyi, anayefahamika zaidi kama Bobi Wine, ameahirisha kampeni zake, kufuatia kujeruhiwa kwa maafisa wake wa kampeni na kuharibiwa kwa gari lake.
Kiongozi huyo wa upinzani amesema risasi zilifyatuliwa kwenye gari lake na kutoboa matairi ya gari lake na kumfanya asiweze kusafiri tena.
Video zilizosambazwa na timu ya kampeni ya Bobi wine kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha kitu ambacho hakikutambuliwa kikilipuka umbali wa mita kadhaa kutoka mahali alipokuwa.
Awali katika eneo la Kayunga, mashariki mwa Kampala, gesi za kutoa machozi zilitumika kuwatawanya wafuasi wake.
Maafisa wanne wa kampeni yake walijeruhiwa, mmoja wao aliyetambuliwa kama producer Dan Magic, alipigwa usoni na mmoja wa polisi wanaowalinda wagombea wa urais waliotolewa na Tume ya Uchaguzi pia alijeruhiwa.
Takriban wiki mbili zilizopita, watu 54 waliuawa wakati wafuasi wa mgombea huyo walipokuwa wakiandamana kudai aachiliwe huru baada ya kukamatwa na polisi katika mkutano wa kampeni akishtumiwa kukiuka masharti ya kukabiliana na janga la corona kwa kukusanya umati wa watu, na baadaye akaachiliwa kwa dhamana.