Bodi ya Klabu ya Ihefu FC itakutana mapema baada ya msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara kumalizika ili kujipanga upya kuelekea msimu mpya ambao wamedhamiria kusajili kikosi cha ‘daraja la juu’.
Ihefu FC imekuwa na msimu mzuri tofauti na miaka ya nyuma ambapo dakika hizi za lala salama ilikuwa kwenye ‘joto’ la kupambana kujinusuru kushuka daraja.
Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Zagalo Chalamila, amesema kikao cha bodi yao kitafanyika baada ya kocha mkuu kuwasilisha ripoti ya msimu huu wa 2022/2023 ambayo itatoa mwongozo kuelekea msimu mpya wa mwaka 2023/24.
Chalamila amesema wamedhamiria kusajili wachezaji watakaoongeza nguvu na kuifanya Ihefu FC iwe timu yenye ushindani na inayoogopewa na klabu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Amesema mbali na kusubiri ripoti, mabosi wa klabu hiyo watakutana na benchi la ufundi kufanya tathimini ya timu yao ambayo iliondolewa katika hatua ya Robo Fainali kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
“Bado hatujapokea mapendekezo yoyote kwa sasa kwa sababu hatujakutana na walimu wetu, tunatarajia kufanya kikao maalumu baada ya mechi ya mwisho ya msimu, kuhusu wachezaji wanaotajwa kuondoka hilo pia tunaliona na kusikia katika mitandao.
Kuhusu Mbegu (Yahya) kutakiwa na Simba SC, hilo halijafika kwetu na kwa sababu mkataba wake unafikia ukingoni mwisho mwa msimu huu tutafahamu nini uamuzi wake, Wadada (Nicholas) naye anahusishwa na Singida Big Stars, pia tunasikia ila tutakapopokea ripoti ya kocha wetu na kuangalia je nyota hao anawahitaji, tutakaa nao mezani ili kuwabakiza,” amesema Chalamila.
Ameongeza wanatarajia kuingia sokoni kufanya usajili ‘mkubwa’ na watawabakiza wachezaji ambao watakuwa kwenye mipango ya kocha kwa sababu wanataka kufanya vyema zaidi katika msimu ujao.
Timu yetu inaendelea kufanya mazoezi kama kawaida, tunataka kuhakikisha tunamaliza ligi kwa heshima, tunazitaka alama sita kutoka katika michezo yote miwili iliyobakia ambayo tutacheza nyumbani,” Chalamila amesema
Ihefu FC iko katika nafasi ya tisa ikiwa na alama 33 na kesho Jumanne (Juni 06) itawakaribisha Geita Gold FC huku ikifunga pazia la msimu kwa kuwavaa Kagera Sugar.