Mwanasiasa Bola Tinubu, ameapishwa rasmi kuwa rais wa Nigeria hii leo Jumatatu akichukua nafasi ya Muhammadu Buhari, jenerali wa zamani ambaye amemaliza muda wake baada ya kuongoza kwa mihula miwili madarakani.
Tinubu mwenye umri wa miaka 71, anatokea anashika madaraka kutoka kwa mtangulizi wake mwenye umri wa miaka 80 wakati taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika likikabiliwa na matatizo ya kiuchumi na mzozo wa kiusalama.
Mara baada ya uapisho huo uliofanyika eneo la Eagle Square katika mji mkuu Abuja, Tinubu amesema, “kama rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Nigeria nitatekeleza majukumu yangu na kuongoza kwa uaminifu kwa kadiri ya uwezo wangu, na kwa mujibu wa katiba.”
Viongozi wa kigeni na wawakilishi waliokuwepo katika sherehe hizo ni pamoja na marais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Paul Kagame wa Rwanda na Nana Akufo-Addo wa Ghana, pamoja na wajumbe kutoka Marekani, Uingereza na China.