Mtendaji mkuu wa klabu ya Borussia Dortmund, Hans-Joachim Watzke amekanusha taarifa za kuwa katika mipango ya kumuachia mshambuliaji kutoka nchini Gabon Pierre-Emerick Aubameyang.

Baadhi ya vyombo vya habari vya nchini Gabon, vimeripoti kwamba mshambuliaji huyo amemthibitishia kocha mkuu wa timu yake ya taifa Jorge Costa, kwamba anataka kubadili mazingira ya soka lake.

Aubameyang kwa sasa yupo sanjari na kikosi cha timu ya taifa ya Gabon ambacho mwishoni mwa juma hili kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Mauritania.

Watzke amesema taarifa hizo, hazina ukweli wowote na mpaka sasa hakuna ombi lolote walilolipokea kutoka kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, la kutaka kuondoka.

Amesema anaamini kipindi hiki, mambo kadhaa ya uzushi yataibuka kama ilivyo kwa Aubameyang ambaye ameanza kuhusishwa na mipango ya kutaka kuihama Borussia Dortmund.

“Aubameyang anataka kuondoka? Hizo ni taarifa za uzushi,” alisema Watzke.

“Hata kama suala hilo litakua na umakini kiasi gani, bado tutafuata taratibu za kupokea ofa kutoka kwenye klabu itakayoonyesha nia ya kumsajili na masuala mengine yatafuata, lakini sio kwa mfumo wa kuzushwa kwa taarifa zisizo rasmi.

“Na nikuhakikishie tu, hatupo tayari kumuuza.” alisisitiza Watzke

Tayari klabu za Manchester United, Arsenal, Chelsea pamoja na Real Madrid zinatajwa kuwa katika mawindo ya kumsajili mshambuliaji huyo ambaye msimu wa 2015-16, alifanikiwa kufunga mabao 39 katika michuano yote aliyocheza.

Serikali yatahadharisha kukauka mito mikuu, yatenga zaidi ya bilioni 100 kupanda miti
Juuko Murshid Asafiri Na Kikosi Cha Uganda Kuelekea Kusini