Meneja wa Klabu Bingwa nchini Hispania FC Barcelona, Xavi Hernandez amesema alimwambia rais wa klabu hiyo Joan Laporta kwamba angependa kuwa na Lionel Messi msimu ujao na akasema anazungumza na mchezaji mwenzake huyo wa zamani mara kwa mara kuhusu uwezekano wa kurejea katika kikosi chake.
Messi mwenye umri wa miaka 35 aliondoka Barca miaka miwili iliyopita, lakini atapatikana kama mchezaji huru msimu huu mkataba wake na Paris Saint-Germain utakapokamilika.
“Kuhusiana na kile ninachosimamia, upande wa mambo ya soka, hakuna shaka kwamba ikiwa Messi atarudi atatusaidia,” amesema Xavi akiiambia Diario Sport alipoulizwa kama Messi kurudi kungekuwa na maana.
“Hilo nimeliweka wazi kwa Rais, hilo sina shaka hata moja kwa sababu bado ni mtu wa tofauti, bado ana njaa, ni mshindi na ni kiongozi.
“Hatuna timu yenye vipaji vya 2010, kwa mfano, Messi analeta nini, analeta kipaji. Ana uwezo wa kutoa pasi ya mwisho, kupiga mipira ya adhabu, kufunga mabao.
“Kwa sababu hiyo, kwangu hakuna shaka kwamba anaweza kuongeza mambo mengi. Lakini inategemea yeye.”
Xavi amesema licha ya kuzungumza na Messi, ambaye alicheza naye wakati wakiwa Barcelona, hajui anachofikiria mchezaji mwenzake huyo wa zamani kuhusu mustakabali wake kwa sasa.
“Ni vigumu kujiweka katika viatu vya mchezaji ambaye ameshinda yote,” aliongeza Xavi.
“Sijui ni mashaka gani anaweza kuwa nayo kuhusu kurejea msimu huu. Labda anaweza kuwa mashaka kwa sababu ni mradi mwingine sasa na kwa sababu wachezaji muhimu ambao alikuwa na uhusiano mzuri nao, kama Sergio Busquets na Jordi Alba, wanaondoka. Sijui, siko ndani ya kichwa chake.
“Kwa uhusiano nilionao naye nadhani nimekuwa wazi sana, mlango uko wazi kwake hapa inategemea na uamuzi wake binafsi.”
Hapo awali ESPN ilifichua kuwa Messi ataondoka PSG baada ya mkataba wake kufikia kikomo mwezi Juni, lakini anatajwa huenda akatimkia Saudi Arabia na Ligi Kuu ya soka ya Marekani lakini Barca, wanajipa matumaini ya kumrudisha Hispania.