Bunge la Zimbabwe limemkingia kifua Rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe asihojiwe kuhusu sakata la upotevu wa mapato ya kiasi cha $15 bilioni kutoka kwenye sekta ya madini.
Mugabe alitarajiwa kufika mbele ya Kamati Maalum ya Bunge inayoshughulikia Madini na Nishati, iliyokuwa ikifanya uchunguzi kuhusu upotevu wa kiaisi hicho cha fedha kwenye mgodi wa madini ya almasi.
Sakata hilo limerudishwa mezani likirejea kauli ya Mugabe kwenye sherehe za siku yake ya kuzaliwa mwaka 2016, aliposema kuwa nchi hiyo imepoteza kiasi cha $15 bilioni kwenye sekta ya madini kutokana na ufisadi ulifanywa na mtandao ambao hakuutaja.
Spika wa bunge hilo, Jacob Mudenda anarushiwa lawama na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kwa madai ya kuzuia uamuzi wa kamati hiyo kumuita Mugabe.
“Kama kamati, tulikubaliana kwamba Mugabe aandikiwe barua na Bunge afike mbele ya kamati kujieleza. Tuliuomba uongozi wa Bunge kufanya hivyo, lakini hadi sasa barua haijaandikwa na inaonekana ni kama Spika ameachana na suala hili,” mmoja wa wanakamati alikaririwa na News Day.
Kiongozi wa kamati hiyo, Temba Mliswa alisema kuwa wanaendelea kusubiri uamuzi wa Katibu wa Bunge, kama atamuandikia barua Mugabe siku za usoni, ingawa hadi sasa hakuna matumaini hayo.
Mugabe alikuwa rais wa Zimbabwe tangu ilipopata uhuru na alishinikizwa kujiuzulu nafasi yake mwaka jana.