Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema chini ya uongozi wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli licha ya changamoto mbalimbali lakini waliazimia kufanikisha ndoto ya siku nyingi ya Taifa hili ya kuratibu na kujenga mtradi wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kitendo ambacho kiliibua shangwe kwa wananchi waliohudhuria tukio hilo.
Rais Samia ameyasema hayo hii leo Desemba 22,2022 mara baada ya kushiriki zoeli la ujazaji maji katika Bwawa hilo huku akiielekeza Wizara ya Uvuvi na Mifugo kuweka mipango thabiti ya ufugaji wa kisasa wa samaki katika na kwamba kwa kuwa lipo ndani ya hifadhi, uvuvi utakaofanyika ni lazima uwe wa kisasa.
Amesema, “Nchi yetu chini ya uongozi wa mpendwa wetu Dkt. John Pombe Magufuli katika awamu ya tano, tukasema liwalo na liwe lakini azma hii ya Mwalimu (Julius K. Nyerere) ya ujenzi wa Bwawa hili la kufua umeme ni lazima tuitekeleze. Kupitia bwawa hili tumejenga daraja kubwa na bora zaidi kuiunganisha mikoa ya kusini, kilichobakia sasa ni barabara.”
Mara baada ya kauli hiyo, Rais Samia amesema, “ Naielekeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi hasa TANROADS, kuandaa mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Chalinze hadi Utete kupitia kwenye dara hilo, njia hiyo itafupisha sana usafiri kati ya mikoa ya kusini na kaskazini mwa Tanzania.”