Aliyekua Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Iran na Misri Carlos Queiroz ametangazwa kuwa Kocha Mkuu wa kikosi cha Qatar, tayari kwa safari ya Fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazopigwa Amerika ya Kaskazini 2026.
Marekani, Mexico na Canada zimeungana kuandaa Fainali hizo, ambazo zinatarajiwa kuwa na mtazamo tofauti, kufuatia kuongezwa kwa timu shiriki kutoka 32 hadi 48.
Shirikisho la Soka nchini Qatar limeingia Mkataba wa miaka minne na Kocha huyo, jukumu kubwa alilopewa ni kuhakikisha Taifa hilo la Mashariki ya Kati linafuzu Fainali za mwaka 2026, huku Bara la Asia likipewa nafasi nane za ushiriki.
Qatar iliyokuwa mwenyeji wa Fainali za 2022, iliishia Hatua ya Makundi baada ya kufungwa michezo yote mitatu, hali ambayo imetoa changamoto kwa viongozi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo kuona kuna umuhimu wa kuwa na kikosi imara kitakachofanya vizuri kwenye Fainali zijazo.
Queiroz aliifundisha Timu ya Taifa ya Iran katika Fainali tatu mfululizo za Kombe la Dunia tangu mwaka 2014, akashindwa kutinga hatua ya 16 Bora.
Queiroz, ambaye atatimiza umri wa miaka 70 itakapofika Machi Mosi, aliwahi kuifundisha timu ya taifa lake la Ureno, wakati wa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, akitokea Hatua ya 16 Bora na Hispania.
Aliifundisha Misri kwa muda mfupi kuanzia Septemba 2021 hadi Machi 2022 akiwaongoza Mafarao hadi Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2021, na mchezo wa mwisho wa mchujo wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2022 kabla ya kushindwa mara zote mbili dhidi ya Senegal.
Qatar chini ya Queiroz ina michuano miwili ya Bara la Asia, ikiwa mwenyeji wa michuano hiyo itakayoanza mwezi Januari 2024. Pia ina Mwaliko wa Fainali za Mataifa ya Amerika ya Kati na Kaskazini ‘CONCACAF’ mwezi Juni 2023.