Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi – CCM, Daniel Chongolo amesema hakuna chama chochote cha Siasa au Mtu yeyote aliye na uhitaji mkubwa wa Katiba iliyo bora na yenye manufaa kwa Watanzania kuliko CCM.
Chongolo, ametoa kauli hiyo alipowasili wilayani Mufindi mkoani Iringa, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku saba yenye lengo la kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025.
Amesema, Wananchi katika eneo hilo wanatakiwa kutokuwa na wasiwasi akisema kazi ya ujenzi wa nchi sio nyepesi na inahitaji watu wote kuwa sawa.
“Nimesikia sikia huko watu wanasema sema kuhusu katiba mpya, labda niwaambie tu kwamba CCM tunahitaji katiba iliyobora kuliko mtu yoyote yule, ndio Maana Chama cha Mapinduzi kimempa ridhaa na dhamana mwenyekiti wake na Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuanzisha mchakato wa mapitio kuhusiana na suala la Katiba mpya” alisema Chongolo.
Katika ziara hiyo, Chongolo ameambatana na Wajumbe wawili wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Katibu wa NEC Oganaizesheni, Issa Haji Ussi (Gavu) na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema.