Mipango na mikakati ya Simba SC kuelekea msimu mpya ni kuona timu yao inafanya vizuri zaidi katika mashindano yote watakayoshiriki baada ya kumkabidhi madaraka ya usajili wa wachezaji Kocha Mkuu, Robert Oliveira ‘Robertinho’.

Robertinho atasaidiana na mtaalam wa kusaka vipaji, Mels Daalder, kuhakikisha Simba SC inakuwa na kikosi imara, kipana na kitakachotimiza malengo yao.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Imani Kajula, alisema baada ya klabu itakuwa makini zaidi katika mchakato wa usajili ambao utazingatia mapendekezo ya Benchi la Ufundi kwa kutorudia makosa yaliyojitokeza msimu unaomalizika.

“Simba SC ni timu kubwa na tumeona tulipokosea msimu uliopita hasa katika aina ya usajili wetu, hilo jambo hatuhitaji kujirudia tena, tunahitaji kufanya usajili mkubwa na mzuri kulingana na wachezaji ambao wamependekezwa na kocha wetu Robertinho, wapo ambao tayari majina yao yapo mezani, tutayafanyia kazi na kujiridhisha kabla ya kufanya uamuzi wa kuwasajili,” amesema Kajula

Ameongeza kupataikana na Mels yalikuwa ni matakwa ya muda mrefu ya klabu katika kuboresha baadhi ya maeneo na kwenda na uongozi wa kisasa.

Afisa huyo amesema kwa kumtumia msaka vipaji huyo ambaye anaijua vyema Simba SC, Ligi Kuu Tanzania Bara na soka la Afrika kwa ujumla, wanaamini watafanikiwa kupata kile ambacho wanakitarajia.

Simba SC inajipanga kujiimarisha baada ya kumaliza msimu huu kinyonge kwa kushindwa kutwaa mataji matatu ya hapa nchini huku pia timu yao ikiondolewa kwa mara nyingine katika mashindano ya kimataifa kwenye Hatua ya Robo Fainali.

Mgunda ajibu dhihaka, kashfa za Ally Kamwe
CCM inahitaji katiba bora, yenye manufaa - Chongolo