Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kimezungumzia kitendo cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kumuomba radhi Rais Samia Suluhu na Watanzania, kufuatia taharuki iliyotokana na kipande cha video kinachomuonesha ‘akipinga’ hatua ya Serikali kuendelea kukopa nje ya nchi.
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo, Ramadhani Maneno amewaambia waandishi wa habari leo, Januari 4, 2022 kuwa kitendo cha Spika Ndugai kuomba radhi ni cha kiungwana na sio kujidhalilisha.
“Kitendo cha Spika Ndugai kujitokeza hadharani na kuomba radhi kwa Rais Samia na Watanzania ni cha kijasiri na kiungwana. Hivyo, ombi langu kwa wana CCM wenzangu na Watanzania kuiamini kauli yake,” amesema Maneno.
Aidha, Maneno aliongeza kuwa anampongeza Spika Ndugai kwa hatua hiyo ya kuomba radhi kwani ndivyo ambavyo CCM inawalea wanachama na viongozi wake.
Jana, Spika Ndugai alizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma na kueleza kuwa kauli yake ilibadilishwa kwa uhariri wa picha uliofanywa na wasio na nia njema.
Alisema katika video yake halisi, hakuna sehemu aliyoikashfu Serikali kuhusu mikopo, bali alikuwa akisisitiza kuchangia pato la taifa kupitia tozo mbalimbali.
Wiki iliyopita, kilisambaa kipande cha video kinachomuonesha Spika Ndugai akizungumza kuhusu jinsi ambavyo Serikali inakopa, na kusikika akisema ‘ipo siku nchi itapigwa mnada’. Kauli hiyo ilizua utata na kusababisha ashambuliwe na baadhi ya watu wakiwemo viongozi.
Kwa upande mwingine, watendaji na viongozi wa Serikali, akiwemo Gavana wa Benki Kuu, Prof. Florens Luoga, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi walifanya jitihada za kufafanua kuhusu deni la Taifa na usimamizi wa mikopo.