Chama cha Mapinduzi (CCM) kimechukizwa na kulaani kitendo kilichofanywa na baadhi ya viongozi wa umoja wa wanawake wa chama hicho Mkoa wa Arusha wakiongozwa na mbunge wa viti maalum, Catherine Magige.
Mbunge huyo jana Alhamisi Mei 27, 2021 alikwenda makaburini yalikokuwa yakifanyika mazishi ya mfanyabiashara Kuzula Madoda inayedaiwa kuwa ni mchumba wake.
Madoda alifariki dunia Mei 24, 2021 na ameacha mke, Aziza Msuya na watoto.
Kitendo cha Catherine kwenda makaburini kiliibua hali ya sintofahamu kutokana na watu waliokuwa naye kuvunja geti na kuingia katika makaburi hayo ya familia.
Taarifa ya chama hicho iliyotolewa na katibu wa itikadi na uenezi, Shaka Hamdu Shaka leo Ijumaa Mei 28,2021 inaeleza kuwa CCM inaheshimu katika kujenga uimara wa familia, kuheshimiana ndani ya jamii na kuendeleza upendo katika familia halali badala ya mivutano na uvurugaji usiokuwa na sababu.
“Chama kinatafakari kwa undani kwa mujibu wa kanuni za maadili na katiba ya CCM, na kuchunguza kwa kina ili kuchukua hatua za kimaadili kwa wote watakaothibitika kuwa sehemu ya matukio yaliyojenga kukiuka kwa katiba, kanuni na utamaduni wa kuheshimu na kuheshimiana uliojengeka ndani ya CCM,” inaeleza taarifa hiyo.