Chama cha Kijamii (CCK) kimepanga kufanya mkutano wake mkuu katika ukumbi ulioko ndani ya Ikulu iliyoko Magogoni jijini Dar es Salaam, Februari Mwakani.

Mwenyekiti wa chama hicho, Constantine Akitanda amesema kuwa mpango huo ni sehemu ya kuitikia mwaliko wa Rais John Magufuli kwa vyama vingine vya siasa na Watanzania wote kutumia kumbi zilizoko Ikulu.

Akitanda amesema kuwa chama chake kilikuwa na mpango wa kufanya mkutano wake wa kawaida ndani ya Ikulu hivi karibuni lakini wameamua kuahirisha na kufanya mkutano mkuu utakaochukua watu takribani 500.

“Tulitaka kuomba ukumbi wa Ikulu kwa ajili ya ya Kikao cha Kamati Kuu wiki ijayo, lakini tukaona kikao hicho kitakuwa na wajumbe wachache tu yaani 30. Sasa tunajipanga kufanya mkutano huo mkuu utakaokuwa na watu 500,” Akitanda anakaririwa na Mwananchi.

Aliongeza kuwa kikao hicho kitatanguliwa na vikao vya Sekretarieti na Kamati ya Utendaji.

 

Hivi karibuni, Rais Magufuli alijibu malalamiko ya baadhi ya vyama vya siasa kuhusu kufanyika kwa mkutano wa CCM ikulu ambapo aliwaalika Watanzania wote akieleza kuwa Ikulu ni mahali pa Watanzania wote.

“Nawakaribisha sana hapa Ikulu ni kwenu. Kwahiyo sioni aibu kuwakaribisha wana CCM, lakini pia kwa Watanzania wote na ndio maana nina wageni kutoka nje wamefika hapa Ikulu, wanamuziki niliwakaribisha hapahapa na wakati wa futari tulifanyia hapa hapa,” alisema Rais Magufuli.

Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM (NEC) ulifanyika katika ukumbi wa Ikulu wiki iliyopita.

RC Rukwa aishauri benki ya NMB kufungua tawi bonde la ziwa Rukwa.
Roma asema kundi la ‘Rostam’ litavunjwa na michepuko