Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Mark Njera amethibitisha kutokea kwa ajali iliyoua watu watano na kuwajeruhi wengine sita baada ya gari la abiria basi aina ya TATA kuacha njia na kuligonga Gari aina ya Isuzu Jane .
Ajali hiyo imetokea jana Septemba 15, majirà ya saa 7 mchana katika kijiji cha Msanga kata ya Mitesa mpakani mwa wilaya ya Masasi na wilaya ya Newala , mkoani Mtwara.
Kamanda Njera amesema basi hilo lilipofika maeneo ya kijiji cha Msanga kata ya Msanga lilikutana na Gari aina ya Isuzu Jane yenye namba za usajili T-311 AER. ambalo lilikuwa likitokea wilayani Newala kuelekea kijiji cha Mchauru kata ya Mchauru wlayani Masasi mkoani Mtwara.
Ameeleza kuwa magari hayo yaligongana uso kwa uso jambo ambalo ilipelekea watu tano kufariki dunia na watu wengine sita kujeruhiwa.
Aidha, Kamanda Njera amewataka madereva wa vyombo vya moto kuwa waangalifu barabarani kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani zinavyowaelekeza.
“Tunaendelea kuwasihi madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria zote za usalama barabarani ili kunusuru maisha ya watu wasio na hatia kama kila dereva akifuata sheria kikamilifu ajali zitapungua,” amesema Kamanda Njera.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya ya Newala na majeruhi walikimbizwa wapo hospitalini hapo.