Gwiji wa Soka nchini England Chris Sutton amemkosa vikali Kiungo kutoka Ureno na Bruno Fernandes kwa kusema hapaswi kuwa nahodha wa Kikosi cha Manchester United, baada ya kipigo cha aibu cha mabao 7-0.
Manchester United ilikubali kichapo hicho Jumapili (Machi 05) kutoka kwa Liverpool, iliyokuwa nyumbani uwanja wa Anfield.
Bruno kwa sasa anakiongoza kikosi cha klabu hiyo kama kaimu nahodha, akishika nafasi ya Beki Harry Maguire ambaye amekuwa na wakati mgumu wa kucheza kwenye kikosi cha kwanza.
Kiungo huyo amekosolewa kwa tabia na mtazamo wake katika mchezo dhidi ya Liverpool, ambao dhahir Manchester United ilionesha kukosa muelekeo na kuruhusu idadi kubwa ya mabao.
Sutton amesema: “Kuna watu ambao wamehitimu zaidi kuwa nahodha,”
“Fernandes si kiongozi wao bora. Kuna wengi wanaofaa zaidi yake, Casemiro akiwa mmoja.”
Hata hivyo Gwiji huyo amempendekeza Beki kutoka Ufaransa Raphael Varane kama chaguo sahihi la kurithi mikoba ya kuwa nahodha wa Manchester United.
Kipigo hicho kilikuja siku saba baada ya Manchester United kushinda Taji la Carabao-kombe ambalo ni la kwanza tangu kuwasili kwa Erik Ten Hag kama Meneja, mwezi Mei mwaka 2022.
Machester United inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na imetinga Robo Fainali ya Kombe la FA, pamoja na hatua ya 16-bora ya Ligi ya Europa.
Enzi zake za kusakata Kabumbu Chris Sutton alizitumikia klabu za Norwich City (1991–1994), Blackburn Rovers (1994–1999), Chelsea (1999–2000), Celtic (2000–2006), Birmingham City (2006) , Aston Villa (2006–2007) na Wroxham (2012).