Klabu ya Southampton, imekuwa klabu ya kwanza ya ligi kuu England (EPL) kuthibitisha kukubali mpango wa kukata mishahara kwa wachezaji wake kutokana na athari ya janga la virusi vya Corona.

Wachezaji wa Southampton, watakatwa mishahara yao ya mwezi Aprili, Mei na Juni, ili kulinda kazi za wafanyakazi wengine wa klabu, ambao wapo hatarini kupoteza kazi katika kipindi hiki ambacho uchumi umeyumba.

Meneja wa klabu, Ralph Hasenhuttl, maofisa wa benchi lake la ufundi na viongozi wa bodi ya klabu, nao watakatwa mishahara yao.

Wakati huo huo Ligi Kuu ya Scotland imesogezwa mbele hadi Juni 10 badala ya Aprili 30 kama ilivyokuwa imeamuliwa mwanzo kutokana na kuendelea kuwepo kwa maambukizi ya virusu vya #Corona.

Rais wa Chama cha soka nchini humo Rod Petrie, amesema uamuzi huo unalenga kuhakikisha usalama wa wachezaji na wadau wote wa michezo wakiwemo mashabiki kwa kuwaepusha na maambukizi hayo.

“Ni lazima tuyatii maagizo ya serikali kwani yanalenga kuokoa maisha yetu. Kwa hali ilivyo, hakuna matumaini kwa timu kurejea mapema kwenye mazoezi”, amesema Petrie.

Wakati ligi kuu ikipangiwa tarehe, ligi za madaraja ya chini kuanzia Championship, League One na League Two, hatma yake inategemea uamuzi utakaofanywa katika zoezi la upigaji kura litakalofanyika kesho, Ijumaa, likihusisha vilabu 42 vinavyohusika.

Visa vya Corona vyaongezeka Zanzibar
Rwanda: Waziri afukuzwa, maambukizi ya Corona yaongezeka