Shirika la Afya Duniani WHO, limesema linarekodi maambukizi mapya virusi vya Corona 350,000 kila siku duniani kote, idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la karibu maambukizi 12,000 ikilinganishwa na rekodi ya mapema wiki hii.
Idadi hiyo inajumuisha maambukizi 109,000 kwa Ulaya pekee ambapo kwa mujibu wa wanasayansi wa Uingereza mlipuko wa vurusi vya corona unaongezeka maradufu kila wiki.
Uhispania hasa ndiyo iliyoathirika zaidi kutokana na maambukizi hayo na tayari Serikali nchini humo imetangaza hali ya dharura katika mji wake mkuu wa Madrid ambao unaongoza kwa idadi ya visa.
Ufaransa tayari imeshashuhudia idadi ya kupindukia ya maambukizi hayo ambapo Jana Ijumaa, zaidi ya maaambukizi 20,000 yaliripotiwa katika kipindi cha saa ishirini na nne, jambo ambalo limepelekea upungufu wa vitanda vya kuwalaza wagonjwa mahututi,
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anakutana na mameya wa miji mikubwa kutafuta ufumbizi wa tatizo hilo la ongezeko la maambukizi.