Zikiwa zimesalia siku kumi na saba pekee kuelekea Uchaguzi mkuu wa Tanzania, kamati ya maadili ya tume ya uchaguzi Jimbo la Mtwara Mjini imekifungia Chama cha Wananchi CUF Jimbo la Mtwara Mjini kufanya kampeni kwa siku kumi kuanzia jana Oktoba 10, 2020.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Jimbo la Mtwara Mjini ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa Mtwara Mikindani, Kanali Emanueli Mwaigobeko amesema kuwa Chama cha Mapinduzi kimelalamikia ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi wa Rais,Wabunge na Madiwani ya mwaka 2020 unaofanywa na Chama hicho.
“Kamati ya maadili ya Uchaguzi Jimbo la Mtwara Mjini baada ya kupokea barua ya malalamiko siku za nyuma imeketi kikao mnamo Oktoba 9 mwaka huu ili kujadili malalamiko hayo ambapo Chama cha CUF kilikiri kuyafanya makossa huku wakisema kuwa walifanya hivyo kwa kuwa kuna baadhi ya vyama navyo vinafanya matukio kama hayo,” amesema Mwaigobeko.
Kamati hiyo imeeleza kuwa mara baada ya kuyapitia malalamiko hayo, utetezi na ushahidi, imeridhishwa kuwa CUF Jimbo la Mtwara Mjini wamekiuka maadili ya Uchaguzi mwaka 2020 kwa kutumia lugha za matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na lugha jambo linalochochea uvunjifu wa amani.
Aidha, msimamizi huyo amewataka wagombea na viongozi wa vyama vya Siasa Jimbo la Mtwara Mjini kufuata maadili na kanuni za Uchaguzi.
”Chama cha CUF Jimbo la Mtwara Mjini kinapaswa kuomba Umma msamaha kwa makosa hayo ya ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi huo wa Rais,Wabunge na Madiwani kwa mwaka 2020” amesema Mwaigobeko.