Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa chanzo cha Katibu Mkuu wake, Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuishi katika Hotel ya Serena kunatokana na kutopewa nyumba na serikali.

Kiongozi mmoja wa CUF ambaye hakutaka jina lake litajwe, alieleza kuwa tangu mwaka 2010, Serikali ilimuahidi kumpa nyumba Maalim Seif jijini Dar es Salaam ili awe anafikia pindi anapokuwa jijini humo lakini haikutekeleza.

Alisema kutokana na hali hiyo, kiongozi huyo amelazimika kukaa katika hotel hiyo kwa ajili ya mapumziko kama alivyoshauriwa na Daktari wake na kwamba ni jukumu la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kulipia gharama zote kwa mujibu wa sheria.

“SMZ ndiyo wenye jukumu la kulipa na si vinginevyo, kwani hata kama kuna viongozi wa SMZ wamepewa nyumba kwa muda wote, lakini Maalim Seif hajapewa, sasa kama unataka kujua kwa undani unaweza kuwauliza viongozi wa Serikali wao ndiyo wenye majibu zaidi,” alisema.

Chumba anachoishi Maalim Seif ndani ya Serena Hotel kina hadhi ya Rais ambacho kwa siku moja hulipiwa $2,801.50 (sawa na shilingi 6,126,180 za Tanzania). Hivyo, kwa siku 7 alizokaa ni shilingi milioni 42.946.

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud alikiri kuwa ni kwa mujibu wa sheria Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawajibika kumlipia gharama zote za Hotel ikiwa ni pamoja na gharama za matibabu kama sehemu ya stahiki zake kama Makamu wa Kwanza wa Rais.  

Aliongeza kuwa Maalim Seif ataendelea kupata stahiki zingine zote hata baada ya kustaafu nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, kama ilivyo kwa wastaafu wengine kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, alisema kuwa kutokana na agizo la Rais Magufuli, Serikali ya Muungano ndiyo itakayolipia gharama hizo zote zilizotajwa.

“Kwa ubinadamu wake Rais Magufuli tunamshukuru sana kwani inaonesha namna gani kiongozi huyo wa Jamhuri ya Muungano alivyo na mapenzi mema  na Zanzibar pamoja na viongozi wake,” alisema Waziri Aboud.

 

FIGC Wakubali Kumuachia Antonio Conte
Ratiba Ya Nusu Fainali Ya Emirates FA Cup Yapangwa