Mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo amewataka viongozi wa Serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea, na badala yake wanatakiwa kuwatumikia wananchi wa Nachingwea kikamilifu.
Moyo amesema hayo wakati wa ziara yake ya kijiji kwa kijiji yenye kauli mbiu isemayo ulipo nipo sema kweli sio majungu ambapo alieleza kuwa hataki kusikia habari za mchakato kwenye utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo ya Serikali.
Aliwataka viongozi kutatua changamoto na kero za wananchi kuanzia ngazi ya kitongoji hadi wilaya hivyo kama kutakuwa na kiongozi hataendana na kasi ya serikali ya awamu ya sita basi akae pembeni awapishe wengine wenye uwezo wa kufanya kazi kwa kasi ya serikali ya awamu ya sita.
DC Moyo ametoa siku saba kwa uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea kuhakikisha wanawapa wazee kadi za matibabu kama ambavyo serikali ya awamu ya sita inavyotaka.
Katika hatua nyingine, Moyo aliwataka viongozi wa TARURA kuwasimamia vilivyo wakandarasi wote ambao wamepewe kazi ya ujenzi wa barabara katika wilaya hiyo ili zijengwe kwa kiwango kinachotakiwa.
Aidha Moyo alimtaka Injinia wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea kuhakikisha miradi yote inajengwa kulingana na thamani ya fedha ambazo zimetolewa na serikali kuu pamoja na Halmashauri kwa faida ya Taifa na Wananchi wote.
Ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kuwa walinzi wa amani ili kuondoa vurugu na migogoro mbalimbali ambayo imekuwa inahatarisha amani Taifa
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Injinia Chionda Kawawa alisema kuwa wamepokea maagizo yote yaliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Nachingwea na watayafanyia kazi kwa faida ya wananchi wa wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla.