Jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku uchomaji wa matairi ambayo yamekuwa yakiharibu miundombinu mingi kama vile barabara ambazo zimejengwa kwa gharama kubwa pamoja na kuleta kero kwa raia wema.
Taarifa ya Kamishna wa Polisi, Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu CP Benedict Wakulyamba iliyotolewa kwa niaba ya Inspekta Jenerali wa Polisi imepiga marufuku uchomaji wa matairi sambamba na Disko toto kote nchini na imeelekezwa kuwa watoto washerehekee chini ya uangalizi wa wazazi au walezi.
Jeshi la polisi limewataka wananchi watakao kuwa wamekusanyika katika fukwe za bahari na maziwa kwa ajili ya kusherehekea sikukuu kurejea majumbani mwao mara ifikapo saa kumi na mbili jioni.
Aidha Jeshi la Polisi limesema limejipanga vizuri kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inaimarishwa kwa kiwango kikubwa kwa kuelekeza makamanda wa Mikoa kuimarisha ulinzi kwenye nyumba za ibada na maeneo mengine ambayo wananchi watakusanyika.
Jeshi hilo pia limetoa wito kwa kila mtanzania kutii sheria kwa hiari kwani hakuna atakaye vumiliwa endapo atavunja sheria.