Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema Utekelezaji wa bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23, kwa Wizara yake utazingatia utekelezaji wa vipaumbele vya wizara na inalenga kuhakikisha rasilimali madini zinanufaisha taifa kiuchumi na kimaendeleo kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya kitaifa.
Amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa vipaumbele vya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2022/2023, Bukombe, Geita.
Amesema katika Mwaka wa Fedha 2022/23, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha bajeti ya jumla ya shilingi 83,445,260,000.00 kwa ajili ya Wizara na Taasisi zake ili kuiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake.
“Bajeti hii ni sawa na ongezeko la asilimia 19.95 ya bajeti iliyopitishwa Mwaka wa Fedha 2021/22,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema vipaumbele ambavyo Wizara imepanga kutekeleza Mwaka wa Fedha 2022/23 ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa; kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuwawezesha wananchi kushiriki uchumi wa madini.
“Vipaumbele vingine ni pamoja na kusimamia na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara na kuendeleza rasilimaliwatu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi,” ameongeza.
Katika maelezo yake amesema utekelezaji wa vipaumbele hivyo utahusisha utekelezaji wa mikakati mbalimbali ikiwemo ya kuanzisha na kusimamia migodi mikubwa na ya kati ya uchimbaji madini ya dhahabu na kinywe(graphite) na madini mengine na kuhakikisha migodi yote mikubwa, ya kati na midogo inaajiri watanzania
“Manufaa ya kufungua migodi hii ni kuongezeka mchango wa sekta katika Pato la Taifa, Uongezekaji wa ajira, na manufaa yatokanayo na uwajibikaji wa kampuni za madini kwa jamii (CSR) na ushiriki wa watanzania katika uuzaji wa bidhaa na utoaji huduma katika shughuli za madini,” Dkt. Biteko amesema.
Aidha Wizara ya Madini ina mkakati mwingine ambao ni kukusanya jumla ya shilingi bilioni 894.3 kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 22.12 ikilinganishwa na shilingi bilioni 696.4 zilizopangwa kwa Mwaka wa Fedha 2021/22.