Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ametoa tahadhari kwa wananchi wote wanaotegesha kwa kupanda mazao kwenye maeneo yanayotakiwa kulipwa fidia na Mgodi wa North Mara baada ya uthamini kukamilika ili kupisha mwekezaji kuendelea na shughuli za uzalishaji.
Hayo yamebainishwa Desemba 5, 2022 na Dkt. Kiruswa alipotembelea maeneo yenye tegesha katika Mgodi wa North Mara uliopo kijiji cha Komalela wilaya ya Tarime Mkoani Mara.
Dkt. Kiruswa ameutaka uongozi wa mgodi wa North Mara kuwasilisha taarifa ya wananchi waliotegesha pamoja na vielelezo vyote kuthibitisha kwamba watu wametegesha baada ya shughuli za uthamini kufanyika chini ya usimamizi wa Serikali.
“Tukishawajua hao na vielelezo vipo taarifa hiyo itakwenda kwa vyombo husika kuhakikisha kwamba wananchi hao waliotegesha wanachukuliwa hatua za kisheria sababu wamevunja Sheria ya kuja kuwekeza katika maeneo yaliofanyiwa tathmini,” ameongeza.
Pia, amesisitiza kuwa uthamini wa mali zote kwa ajili ya kupisha maeneo hayo kwa ajili ya uchimbaji madini tayari umefanyika kwa mujibu wa Sheria na Kanuni.
“Wapo baadhi ya wananchi wameshalipwa fidia na wengine wameendelea kubaki kwa madai kwamba fidia waliyopewa haitoshi na wakati uthamini ulipofanyika walikubali na kusaini na wengine wakalipwa,” amesema Dkt. Kiruswa.
Hata hivyo, ameagiza wananchi wote wenye madai kuandika vitu vyote wanavyodai na kuwasilishwa katika Ofisi ya Madini mkoa wa Mara kwa lengo la kufanya uhakiki ili kuendelea na mazungumzo kwa ajili ya kupata haki stahiki.
Aidha, Dkt. Kiruswa pia amesimamisha shughuli za uchimbaji katika kijiji cha Nyabichune baada ya kubaini baadhi ya wananchi kuendelea na shughuli za uchimbaji kinyume na utaratibu licha ya kupewa katazo na Serikali kwenye maduara yaliyo ndani ya makazi ya nyumba zao ambayo baadhi yao wameshalipwa fidia na wengine wamegoma kwenda kuchukua fedha zao baada ya uthamini kukamilika.
Naye, Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara Victor Tumaini amesema kuwa, mgodi upo tayari kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wote katika maeneo wanayohitaji kwa shughuli za uzalishaji na kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kimetengwa kulipa fidia wananchi wote waliofanyiwa uthamini.
Ziara hiyo, imehudhuriwa na Wataalamu kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime na wadau mbalimbali wa Sekta ya madini katika mkoa wa Mara.